Nimekuwa nikisoma sehemu mbalimbali maoni ya watu kuhusu biashara ya mtandao (Network Marketing). Wapo wengi ambao wamethubutu hata kuandika na kuelezea kuwa hii si biashara ya kweli na wakati mwingine wakitumia lugha isiyo ya kistaarabu kabisa. Kutokana na hili nikaona na mimi nitafiti kuhusu mada hii na kujua nini chanzo cha watu wengine kubeza wakiwaona wenzao wanashiriki kwenye biashara hizi. Nimepeleleza chanzo cha biashara hii, nikatafiti ni nini watu mashuhuri ulimwenguni wanasema kuhusu biashara hii na kujaribu kuona sababu zinazowafanya wengine kuona kuwa hii si biashara ya kweli. Naamini kabisa kwa kusoma hapa leo, utajua ni nini hasa kinachoendelea kuhusu biashara hii.
Biashara ya mtandao ipo hapa nchini kwa muda mrefu kidogo na kila siku kampuni mpya za biashara hii zinaingia. Lakini hasa biashara ya mtandao ni nini? Maana kuna wengine hata DECI wanaiita kuwa ilikuwa biashara ya mtandao. Moja ya machapisho niliyoyapenda yanasema hivi kuhusu biashara ya mtandao:
Biashara ya mtandao ni shughuli endelevu ya kujenga mtandao wa watu wanaotumia bidhaa fulani au huduma fulani na kuwashirikisha marafiki, ndugu na watu wengine wanaopenda kujenga mitandao yao. Kadiri mtu atakavyokuwa anawashirikisha watu wengi zaidi na zaidi, ndivyo mtandao wake utakavyokua. Mtu atalipwa kutokana na mauzo anayoyafanya yeye binafsi na kutokana na mauzo ya watu aliowashirikisha na kuwafunza kwenye mtandao wake.
Baada ya kupata ufafanuzi wa neno “biashara ya mtandao”, nafikiri umeelewa katika kampuni zilizoingia hapa kwetu, zipi ni au zilikuwa za mtandao na zipi si au hazikuwa za mtandao.
Kwa sababu biashara hii ipo katika nchi nyingi ulimwenguni, zilizoendelea na zinazoendelea, kuna watu mashuhuri wengi ambao wameizungumzia biashara hii. Moja wa watu hao ni aliyekuwa raisi wa Marekani, Bill Clinton. Unaweza kuona ni nini alikizungumza kuhusu biashara hii alipoona wamarekani wengi walikuwa wanajihusisha na biashara hii. Nimeweka video yake hapa chini:
Mfanyabiashara maarufu ulimwenguni anayemiliki kampuni ya Microsoft, Bill Gates, naye pia alisema haya:
“If I would be given a chance to start all over again, I would choose NETWORK MARKETING.”
Mtu mwingine niliyemweka hapa ni ndugu Robert Kiyosaki ambaye alifanya mahojiano na mwanadada mmarekani mweusi, Oprah, na kueleza kwa nini watu wote wanatakiwa kufanya biashara ya mtandao. Robert Kiyosaki ni mfanyabiashara wa Marekani, mwandishi, mchambuzi wa masuala ya fedha, msemaji kwenye vituo vya redio na mtoa mada za motisha kwa watu wanaohangaika kupata mafanikio katika maisha. Ndugu huyu ana video nyingi sana kuhusu somo letu la leo, lakini leo naiweka moja tu hapa:
Hadi sasa hivi biashara ya mtandao ni biashara yenye thamani ya zaidi ya pound bilioni 170. Watu zaidi ya milioni 90 wanajihusisha na biashara hii na maelfu ya watu hujiunga kila mwaka. Ni biashara inayokua kwa haraka sana na wataalamu wanasema si punde itakuwa ndiyo biashara kuu. Hebu sasa tutazame biashara hii ilianza lini, kivipi na wapi na tuone ilikua vipi na hadi leo hali ni ipi.
Historia Ya Biashara Ya Mtandao
Kwenye miaka ya 1930, kuna mtu aliyejipatia jina kubwa sana, naye aliitwa Carl Rehnborg. Akiwa China kati ya 1917 na 1927, alielezewa umuhimu wa kutumia virutubishi vya kiada kwenye milo na faida zilizotokana na matumizi ya virutubishi hivyo.
Aliporudi Marekani alianzisha kampuni iliyoitwa The California Vitamin Company. Mwaka 1939 alibadilisha jina la kampuni hiyo na kuiita Nutrilite. Katika miaka 6 ya biashara yake alibadilisha mfumo wa biashara yake na kubuni mfumo wa biashara wa Multi Level Marketing ili kuongeza mauzo ya bidhaa zake. Multi level marketing ni jina jingine linalotumika kuelezea biashara ya mtandao (Network Marketing).
Mwelekeo ulibadilika pale washauri wa biashara wawili, Jay Van Andel na Rich DeVos walipojiunga na Nutrilite na kuona nguvu kubwa ya mfumo huu wa biashara, kwani mauzo yaliongezeka kwa kiwango cha kustaajabisha. Wakaunda kampuni yao iliyoitwa Amway na kununua hisa za Nutrilite mwaka 1972. Mwaka 1994, Amway ilimiki hisa zote za kampuni ya Nutrilite na hadi leo ni moja ya makampuni makubwa ulimwenguni.
Muundo Wa Biashara Ya Mtandao Upoje?
Biashara ya mtandao ni namna nyingine tu ya kumfikishia bidhaa mlaji. Biashara za zamani zilimfikishia mlaji bidhaa kutoka kiwandani kupitia kwa muuzaji wa duka la rejareja. Mara nyingi palikuwa na duka la jumla na ajenti kabla ya kufika kwenye duka la rejareja.
Katika mfumo wa biashara ya mtandao kuna tofauti kwa kuwa bidhaa kutoka kiwandani humfikia mlaji moja kwa moja hivyo kuondoa gharama za mwenye duka la jumla na la rejareja. Kampuni sasa huchukua pesa ambayo ingetumika katika matangazo kuwalipa wanachama wao kwa kuwa mapromota wa bidhaa zao. Nafikiri utaona wazi kuwa hii ni njia safi zaidi ya kufanya biashara.
Jee, Biashara Ya Mtandao Ni Pyramid?
Kuna baadhi ya watu utawasikia wakisema biashara ya mtandao ni pyramid scheme. Ukweli ni kwamba, Hapana. Pyramid scheme ni biashara inayofanywa bila kuwepo bidhaa ya kuiuza, au kutaja bidhaa ambazo hazieleweki au ambazo zina bei za juu na haziuziki kirahisi. Kwenye pyramid scheme, pesa mara nyingi huwa ndiyo bidhaa. Biashara za Pyramid Schemes hukatazwa kisheria.
Unaweza kutofautisha biashara halali ya mtandao na pyramid schemes kwa kutazama mkazo unaowekwa kwenye biashara. Wakati kampuni ya mtandao ina bidhaa ambazo zimeuzwa kwa kipindi kirefu na kuwasadia watu wengi, pyramids huweka mkazo kwenye kusajili watu wajiunge na kampuni na kusisitiza kupewa mafao kutokana na uwingi wa watu uliowasajili na si bidhaa utakazouza. Pyramids hutoa matangazo ya kupata pesa nyingi na kwa muda mfupi sana na kukuahidi kukupandisha ngazi kulingana na idadi ya watu utakaowasajili.
Biashara ya pyramid hutaka uwekeze kiasi kikubwa cha pesa ili usajiliwe nao tofauti na biashara halali za mtandao.
Aina moja ya Pyramid schemes ni Ponzi scheme. Ponzi scheme ni uwekezaji wa kijanja unaolenga kuwaibia watu kwa kuwalipa wanachama waliopo kupitia pesa inayotolewa na wanachama wapya na kuleta picha ya kupata mafao na faida wakati hakuna kitu. Wenzetu wanaita the “rob Peter to pay Paul” principle.
Jina hili lilitolewa baada ya Charles Ponzi aliyejenga mtandao mkubwa huko Uingereza na kuwalipa watu waliotangulia pesa nyingi kutokana na pesa za watu waliojiunga baadaye. Alilipa faida kubwa ya asilimia 40 katika siku 90 tofauti na asilimia 5 iliyokuwa ikitolewa na benki. Baada ya wageni kupungua kujiunga na mtandao wake, alishindwa kuendelea kuwalipa watu na mfumo wake ulikufa. Alifungwa jela kwa kuwalaghai watu kwenye miaka ya 1920.
waka 2008 mtandao mkubwa wa ponzi scheme uligundulika, mtandao huo uliendeshwa na Bernard Madoff. Mtandao huu uliwaibia watu kiasi cha dola bilioni 65 katika kipindi cha miaka 17 na kuufanya kuwa mtandao mkubwa zaidi wa ponzi scheme kuliko yote katika historia.
Kwa Nini Biashara Ya Mtandao Ni Biashara Ya Karne Ya 21?
Sababu kubwa ya kufumka kwa biashara ya mtandao ni ukosefu wa kuwa na uhakika katika ajira, watu wengi wanaanza kuliona hilo; na, upatikanaji wa ajira kila siku unazidi kuwa mgumu. Idadi ya watu duniani kila siku inaongezeka kwa haraka sana kuongezea ugumu wa upatikanaji wa ajira.
Watu wenye maono ya mbali na kuihisi hali halisi, wameanza kuchukua hatua na wanajiunga na biashara ya mtandao. Miaka 50 ijayo itaonyesha wimbi jipya la mamilionaire kutoka biashara ya mtandao. Sasa hivi, wachache tayari wameanza kujichomoza.
Katika mada nyingine tutajadili faida 10 za biashara ya mtandao. Hadi hapo tunakutakia usomaji mwema. Usisite kutoa yako ya moyoni kuhusu mada yetu ya leo, ni furaha kwetu kuupata mchango wako.
Tafadhali tembelea blog yetu kujisomea mada mbali mbali zinazohusu biashara za mtandao na fursa za kufanya biashara za mtandao zinazotolewa na kampuni za Green World TanzanianaTrevo Tanzania Ltd. Humo unaweza kuona wasomaji wengine wana maoni gani kuhusu mada zetu tunazoziandika. Pia unakaribishwa kuona video mbali mabali zinazohusu biashara ya mtandao ya kampuni ya Green World kwenye channel yetu ya YouTube.
Kutembelea blog bofya HAPA.
Kutembelea channel yetu ya YouTube bofya HAPA.
Laurian.