Vitu Muhimu Vya Kuzingatia Ili Ufanikiwe Katika Biashara Ya Mtandao

MWANACHAMA SAFARINI KIBIASHARA
MWANACHAMA SAFARINI KIBIASHARA

Biashara ya mtandao ni mfumo wa biashara ambao unamlipa mwanachama aliyejiunga na kampuni husika kutokana na mauzo yake binafsi na mauzo ya wanachama ambao mwanachama huyo aliwashawishi wajiunge na biashara ya kampuni hiyo. Katika ukurasa huu, tutajifunza jinsi ya kupata mafanikio katika biashara hizi  za mtandao.

Biashara ya mtandao inatoa fursa kwa mwanachama kupata malipo endelevu (residual income) bila ya yeye kujihusisha katika mauzo. Malipo endelevu ni malipo ambayo mwanachama anapata kutokana na kazi aliyoifanya mara moja na akaendelea kupata malipo muda mrefu baadaye bila yeye mwenyewe kuhusika moja kwa moja. Mfano ni pale mwanachama anapomwingiza mwanachama mgeni katika kampuni fulani na mwanachama huyu mgeni akanunua bidhaa iitwayo X.

Huyu mwanachama mgeni akiipenda bidhaa hii na akatoa oda ya kuipata kila mwezi, mwanachama aliyemwingiza mgeni huyu ataendelea kulipwa bonasi inayotokana na mauzo ya bidhaa hiyo mwezi ule alipomwingiza mgeni huyu na ataendelea kulipwa kila mwezi baadaye ili mradi mwanachama huyu mgeni anaendelea kutumia bidhaa X. Ulipwaji wa bonasi hii bila wewe kujishughulisha tena unakupa kipato bila wewe kufanya kazi tena (passive income). Ukiwa umeweza kuwasajili chini yako wanachama wengi wa namna hii, basi tayari utapata kipato endelevu kikubwa kila mwezi.

Biashara ya mtandao inakupa pia fursa ya kupata kipato kutokana na vizazi mbalimbali chini yako. Wale wanachama uliowasajili wewe na kuwafundisha jinsi ya kufanya kazi, ni kizazi chako cha kwanza. Wanachama wa kizazi chako cha kwanza nao watawasajili ndugu zao, rafiki zao na watu wengine na kuwaelekeza jinsi ya kufanya mauzo ya bidhaa za kampuni yenu. Vivyo hivyo, hawa waliosajiliwa na wale uliowasajili, watawasajili ndugu, jamaa na rafiki zao. Kwa mtindo huu, utakuwa umejijengea mtandao wa watu chini yako wanaofanya biashara ya kampuni yako.

Hii ndiyo maana ya biashara ya mtandao. Wale waliosajiliwa na wanachama wa kizazi chako cha kwanza, watakuwa wanachama wa kizazi chako cha pili na hivyo kuendelea na vizazi vingi chini yako. Kampuni itakulipa kutokana na mauzo yanayofanywa wanachama wa vizazi vilivyo chini yako. Kila kampuni ina utaratibu wake kuhusu idadi ya vizazi vilivyo chini yako vitakavyolipwa. Kampuni nyingine, hazina ukomo wa idadi ya vizazi vilivyo chini yako vitakavyokupa malipo.
Biashara ya mtandao inakulipa kutokana na kazi ya wanachama uliowasili wewe binafsi na wanachama waliosajiliwa na wale uliowasajili na vizazi vilivyo chini yako. Hapa unapewa kipato kutokana na mwendelezo wa nguvu zako za kusajili na mwendelezo wa maelekezo uliyoyatoa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine (leveraged income).

Ili Kufanikiwa Katika Biashara Ya Mtandao Fanya Yafuatayo

Awali ya yote inabidi nieleze na kutoa mkazo kuwa biashara za mtandao ni kufanya kazi na watu na kuwafundisha jinsi ya kubadilika na kupata kipato kufikia viwango vya juu. Kitu kikubwa ni kujifunza na kutumia mbinu bora za kujenga timu chini yako. Ukisha kuwa na kikosi ambacho umekifundisha vizuri, kitafanya kazi na kukufanya uongeze kipato chako kila mwezi. Unaanza na kuwafundisha wale ambao umewasajili wewe binafsi, nao watawafundisha waliowasajili na zoezi hilo kujirudiarudia na hatimaye kupata kikosi bora kinachofanya kazi. Kampuni nyingi za mtandao zinatoa mafunzo na kutoa nyenzo za kusaidia katika kutoa mafunzo.

Sasa ili uweze kupata mafanikio kwenye biashara za mtandao, pitia kwa makini na tekeleza yafuatayo:

Chagua Vizuri Kampuni Yako Ya Mtandao

Kwangu mimi binafsi, hili ni la maana kuliko mengine yote ambayo tutayajadili hapa chini kwa sababu ikiwa utaangukia mikononi mwa kampuni mbovu, haya yote tunayoyajadili kwenye mada hii hayatakusaidia, hata kama utatumia nguvu na mbinu za namna gani. Zingatia yafuatayo katika kuchagua kampuni yako ya kufanya nayo biashara:

  1. Sifa Za Kampuni: Chunguza sifa za mmiliki wa kampuni unayotaka kujiunga nayo na historia ya kampuni kwa ujumla. Jee, kampuni ina anwani ya kudumu? Kampuni iliyo kwenye biashara hii kwa muda mrefu, itakuwa na uhakika zaidi katika shughuli zake. Chunguza vile vile katika kipindi ambacho kampuni imekuwa ikifanya kazi imekuwa na rekodi gani. Jee, imewaingiza wanachama kwenye migogoro ya aina yo yote? Kuna wanachama ambao wametajirika na kampuni hiyo? Inakua kibiashaara, imefikia ukomo au inateremka kibiashara? Jiunge kwenye kampuni ambayo majibu yake kwa maswali hayo ni mazuri.

2. Ubora Wa Bidhaa Au Huduma Za Kampuni: Mteja ye yote yule atanunua bidhaa ya kampuni au atapenda kupata huduma za kampuni pale tu ambapo amepata sifa kuwa bidhaa za kampuni hiyo au huduma ya kampuni hiyo itamsaidia kuondoa matatizo aliyo nayo na si kinyume cha hilo. Kampuni yenye bidhaa nzuri au huduma nzuri itakupunguzia kazi ya kufanya matangazo au kutoa maelezo badala yake utapata wateja wengi walioelekezwa kwako (referrals) na kupata faida kubwa.

3. Mpango Mzuri Wa Malipo (Good Compensation Plan): Mpango wa malipo wa kampuni unayofanya nayo kazi ndio utakaosema wewe kama mwanachama utapata kiasi gani kutokana na kazi uliyoifanya. Kwa vile ulijiunga ili upate kipato kizuri, haina maana kujiunga na kampuni ambayo haina mpango mzuri wa malipo. Ni vizuri kujiunga na kampuni ambayo ina mpango wa malipo unaoeleweka kiurahisi, unaotekelezeka na unaolipa vizuri.

4. Msaada Wa Mafunzo Na Nyenzo Za Kazi: Kampuni inayotoa mafunzo ya bure kwa wanachama wake, vipeperushi na vifaa vingine vya kusaidia kufanya kazi itakusaidia kufikia malengo yako ya kupata kipato kikubwa kwa muda mfupi zaidi. Kampuni iliyo bora itatoa njia nyingi za kutoa msaada, namna nyingi za kuweza kujifunza kuhusu biashara yake, mabango, tovuti binafsi na vitu vingine ili uweze kupanda kiurahisi na kufikia malengo yako.

Ielewe Vizuri Kampuni Yako

Chukua muda wa kutosha kujifunza kuhusu mpango wa malipo wa kampuni yako, kampuni nyingine zina vitu vingi sana ambavyo ungeweza kuvifanya. Ukisha pata undani wa kampuni, amua njia yako utakayoifuata (your personal philosophy) katika kufikia malengo yako katika biashara ya kampuni hiyo. Pata ushauri kila mara kutoka kwa watu walio juu yako ili ujue njia walizozitumia kufanikiwa katika biashara ya kampuni hiyo.

Ongoza Timu Yako Vizuri

Wanachama wapya kwenye kampuni wanahitaji msaada kama vile ulivyohitaji wewe wakati unaanza biashara na kampuni hiyo. Hakikisha unatoa muda wa kutosha kuwafundisha kuhusu biashara yenu, washike mkono hadi pale watakapoanza kumudu kuifanya biasharaa hiyo wenyewe. Kumbuka kuwa kufanikiwa kwa walio chini yako ndiyo mafanikio yako. Kusajili wanachama chini yako kisha kuwaacha yatima hakutakusogeza po pote katika biashara yako.

Tumia Vizuri Mtandao

Kwa wakati tulio nao sasa, hakuna chombo bora cha kufanyia matangazo ya biashara yako zaidi ya matumizi ya mtandao (internet). Unaweza kutumia mitandao ya kijamii (social media sites), ukajenga blog au tovuti kwa ajili ya kuitangaza biashara unayoifanya. Mitandao ya kijamii yote mikubwa – Facebook, Google+, Instagram, Tweeter  n.k. – inaruhusu watu kufungua akaunti bure na kutangaza biashara zao bure kabisa. Baadhi ya mitandao inaruhusu kufungua kurasa za kibiashara, kwa mfano, Fan Page kwenye facebook, ambamo utajenga urafiki na watu mbalimbali ambao wataelewa ni biashara gani unaifanya.

Panga Muda Wa Kujiendeleza

Mafanikio katika biashara ya mtandao yameonekana kuendana na ukuaji wa kiwango chako wewe binafsi kifikra na kiutendaji.

Uchu wa kujifunza, kujiendeleza binafsi na kukua binafsi.

Hapo juu ndilo neno kuu katika kipengele hiki  cha kukusaidia kukua kibiashara. Watu wote waliofikia mafanikio makubwa walisikiliza kanda za kaseti, walisoma vitabu na walihudhuria semina. Walitenga kipande cha siku kwa ajili ya kujiendeleza binafsi, Na, inaonekana kuwa, kadiri walivyopata mafanikio zaidi -ndivyo walivyotenga muda zaidi kwa ajili ya kujiendeleza.

Imebainishwa kuwa kama  unataka kufika kiwango fulani, au kulifikia lengo fulani -lazima ufikie kuwa ni aina ya mtu ambaye amefikia kiwango hicho au amefikia lengo hilo. Vipawa vimejificha ndani yako, vikingojea kuamshwa. Unachotakiwa kukifanya ni kuviibua.

Chagua watu wachache waliofanikiwa katika biashara hii na sikiliza mikanda yao ya  video au soma vitabu walivyoviandika. Mimi napenda kuwasikiliza na kusoma vitabu vya Jim Rohn, Eric Worre na Randy Gage.

Jee, una mbinu ambazo umezitumia kufanikiwa katika biashara ya mtandao ambazo hazijatajwa hapa na ungependa kuwafahamisha wasomaji wengine? Usisite kutuandikia.

Baada ya kuisoma mada hii, katika mada nyingine tutazungumzia moja ya kampuni bora za mtandao Tanzania, kampuni ya  Green World Tanzania.

Laurian.